Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, sambamba na kuendelea mgogoro wa kibinadamu huko Ghaza na kuongezeka wasiwasi wa kimataifa, ujumbe rasmi wa Cuba ulioshiriki kwenye mkutano wa UNESCO huko Samarkand ulitoa msimamo ulio wazi. Wawakilishi wa Cuba, walioshiriki katika kamati za elimu, fedha na masuala ya utawala, walisisitiza umuhimu wa kulinda haki ya elimu, utamaduni na hadhi ya kibinadamu katika ardhi zinazokaliwa kimabavu na Israel.
Katika taarifa iliyosomwa na ujumbe wa Cuba, ilielezwa kwamba: “Muda wa kuwa taifa la Palestina halijafanikiwa kuunda nchi huru ndani ya mipaka yake kabla ya mwaka 1967 mji mkuu wake ukiwa Jerusalem Mashariki, hakutakuwa na amani ya kweli na ya kudumu.”
Msimamo huu, uliongezwa, ni mwendelezo wa siasa ya muda mrefu ya Havana ya kuunga mkono harakati za ukombozi na za haki duniani kote.
Wawakilishi wa Cuba walirejelea ripoti za UNESCO zinazohusiana na uharibu wa mamia ya shule na kuumizwa maelfu ya wanafunzi na walimu wa Kipalestina, na wakasisitiza umuhimu wa kuliunga mkono Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) na miradi yake ya kielimu huko Ghaza.
Aidha, Cuba ilikumbushia ushirikiano wa muda mrefu wa kielimu kati yake na watu wa Palestina, ikibainisha kuwa kila mwaka mamia ya wanafunzi wa Kipalestina, hasa katika taaluma za udaktari na sayansi za kijamii, husoma katika vyuo vikuu vya nchi hiyo.
Ziara ya hivi karibuni ya Rais Miguel Díaz-Canel kwa kundi la wanafunzi wa Kipalestina katika Kasri la Mapinduzi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Cuba, ni ishara ya urafiki wa kihistoria na uhusiano wa kibinadamu kati ya mataifa hayo mawili.
Ujumbe wa Cuba ulionya pia kuhusu kuenea kwa ukiukwaji wa sheria za kimataifa, na kuiomba UNESCO ichukue jukumu hai zaidi katika kulinda elimu na kujenga upya tamaduni katika maeneo yaliyoathiriwa na vita, huku ukisisitiza kwamba: “Elimu si chombo cha maarifa pekee, bali ni nguzo kuu ya upinzani dhidi ya ukaliaji na udhalilishaji wa mataifa.”
Mwisho wa taarifa hiyo, Cuba ilisisitiza kujitolea kwake kwa umoja wa kimataifa, haki ya dunia, na haki ya mataifa kujitawala, na ikazihimiza nchi zote zichukue msimamo wa kibinadamu – si wa kisiasa tu – katika kuwatetea watu wa Palestina.
Maoni yako